Dibaji ya Qurani Karimu

Kila sifa njema zinamstahikia Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote, na rehema na amani zimshukie Mtume Muhammad (SAW) na watu wake na wafuasi wake wanaomfuata kwenye uongofu aliokuja nao mpaka Siku ya Kiyama.

Qurani Karimu ni Kitabu cha Mwenyezi Mungu na Wahyi wa mwisho alioteremshiwa Mtume Muhammad (SAW) kwa ajili ya kuwaongoza wanadamu kutokana na giza la upotofu na ushirikina kuwatia kwenye mwangaza wa imani ya Mwenyezi Mungu Mmoja usiozimika nuru yake, na kwenye uongofu wa daima utakaowanawiria maisha yao na kuyafanya kuwa mazuri na ya furaha hapa duniani na kesho Akhera.

Mwenyezi Mungu, tangu alipoiteremsha hii Qurani aliwawafikia watu wengi kuisoma na kuihifadhi na kuifasiri na kuzishughulikia elimu zenye uhusiano na Kitabu hiki kitukufu, na Waislamu wa makabila mbali mbali waliingia kundini kuifasiri Qurani kwa lugha zao ili watu wao waweze kuifahamu na kuizingatia na kuitumia katika maisha yao, na leo alhamdulillahi kuna tafsiri za Qurani za lugha tofauti tofauti kote ulimwenguni.

Kutokana na juhudi hii kubwa iliyofanywa na watu wa makabila mbali mbali, leo Waislamu hawana taabu ya kuifahamu Qurani ambayo ni desturi ya maisha yao na muongozo wa mambo yao yote hapa duniani. Bidii hii imewasahilishia Waislamu wengi kuyafahamu Maneno ya Mola wao na kujaribu kufuata maelekezo yaliyokuwemo humo ya kufanya mema na kujiepusha na maovu na kuzingatia maonyo yaliyokuwemo kuhusu wale walioasi ambao mwishowe waliangamizwa.

Lugha ya Kiswahili inayozungumzwa na mamilioni ya watu wa Afrika Mashariki, kadhalika imepata hadhi ya kufasiriwa Qurani Karimu kwa lugha hio na leo alhamdulillahi kuna tafsiri mbili kamili kwa lugha ya Kiswahili za wanazuoni wa Afrika Mashariki, Sheikh Abdallah Saleh Farsy na Sheikh Ali Muhsin Al-Barwani waliotangulia mbele ya Mola wao, Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema, amin.

Tunamuomba Mola aliyetukuka anipe na mimi nguvu na uwezo na tawfiki kuongeza tafsiri yangu hii inayoitwa “Qurani Karimu” katika maktaba ya Kiislamu ya vitabu vya Kiswahili ili ije kuwafaa na kuwanufaisha Umma wa Kiislamu unaozungumza kwa lugha hii. Inshallah tafsiri hii itakuwa nyongeza ya juhudi ya wanazuoni waliotutangulia na Mwenyezi Mungu atatupa sote pamoja na wale wenye kunufaika na tafsiri hizi thawabu nyingi na ujira mkubwa kwa kuzisoma, amin.

Kwa ufupi, tafsiri hii ya Qurani Karimu imefaidika sana kutokana na tafsiri za Maulamaa wakubwa wa tafsiri za Kiarabu na wafasiri wa Qurani wa lugha ya Kiingereza, na kadhalika wafasiri waliotangulia wa lugha ya Kiswahili, na kwa hivyo asione ajabu mwenye kuisoma akakuta baadhi ya tofauti katika tafsiri, kwani tangu wakati wa mwanzo, Masahaba walitafautiana katika kufasiri baadhi ya Aya, na hili ni wazi kwa yule mwenye kuzisoma tafsiri za Maulamaa wakubwa wa Kiarabu.

Wallahu Waliyut-Tawfiq.

The Holy Quran contains:

Juz'u
0
Hizb
0
Surah
0
Ayah
0

Tafsiri tulizozitumia kufasiri Qurani Karimu

Katika muda wa zaidi ya miaka kumi nilishawishika sana na fikra ya kuifasiri Qurani Karimu kwa lugha ya Kiswahili, si kwa kutokuwepo tafsiri hizi kwa lugha hio, lakini zaidi ni kujaribu kuzidi kufafanua yale yaliyokuwemo katika Kitabu hiki Kitukufu cha Mwenyezi Mungu ambacho daima kina hazina mpya zilizozikwa ndani yake zinazongojea Waislamu kuzitafuta na kuzidhihirisha.

Baada ya kuzisoma tafsiri kadha wa kadha za lugha ya Kiarabu na Kiingereza na Kiswahili na kuzipitia mara kwa mara katika masomo yangu ya lugha ya Kiarabu na Sharia, na katika juhudi yangu ya kufasiri baadhi ya vitabu vya Kiislamu, na kwa kuhudhuria kwangu darsa za tafsiri ya Qurani za wanazuoni mbali mbali, Unguja na Mombasa, nilizidi kukinaika na kuingiwa na hamu na hima na hamasa ya kutaka 

kuzama kwenye Kitabu hiki cha Mola wa walimwengu wote ili na mimi nipate sehemu yangu ya kukihudumikia Kitabu hiki Kitukufu na kupata thawabu na radhi za Mola wangu kwa kusimama katika mstari wa mbele pamoja na wale waliopitisha juhudi kuifikisha nuru yake hii kwa Umma wa Kiislamu.

Mwenyezi Mungu aliyetukuka aliniwafikia kupata nafasi ya kusoma tafsiri mbali mbali ambazo zilinawirisha kuhusu Qurani Karimu na madhumuni yake na elimu zake tofauti tofauti na makusudio makubwa ya kuteremshwa Kitabu hiki Kitukufu kiwe ndio Kitabu cha mwisho cha uongofu wa wanadamu wote ulimwenguni.

Vitabu vya tafsiri vya Maulamaa wafuatao wa elimu hii vilinisaidia kuzidi kufahamu elimu hii na kuniwezesha na kunisahilishia kazi yangu ya kufasiri Qurani Karimu kwa lugha ya Kiswahili. Tunamuomba Mola wa walimwengu tawfiki na qabuli, amin.

Tafsiri za Kiarabu

Tafsiri za Kiingereza

Tafsiri za Kiswahili